Mchezo wa Kukata Kiuno

sábado, 17 de março de 2012

Njia ya kutafuta na kupata kazi kirahisi

Kuishi muda mrefu bila kuwa na kazi kuna madhara mengi kisaikolojia, watu wengi hupatwa na vichaa na wengine, kujiingiza katika ulevi wa kupindukia, utumiaji dawa za kulevya na uhuni kutokana na kukata tamaa ya maisha hasa wanapopoteza kazi au wanapomaliza masomo na kukosa ajira walizokuwa wakizitazamia.

Hii inatokana na watu wengi kukosa elimu ya namna ya wanavyoweza kutumia vizuri muda wao wa dhahabu wanapokuwa hawana kazi. Unaitwa muda wa dhahabu au ‘Unemployment golden time’ kwa sababu mkosa ajira huathirika endapo atashindwa kutumia muda wa awali kujiokoa na makucha ya kukosa kazi.

Wataalamu wa masuala ya ndege wanaziita sekunde 90 za awali baada ya ndege kuanguka kuwa ni “golden time” kwa sababu ndizo ambazo mtu anaweza kuzitumia kujiokoa, vinginevyo hali huwa mbaya na pengine kuna uwezekano mdogo wa wahanga kutoka salama baada ya dakika hizo kupita.

Hivyo basi maisha bila ajira nayo yana muda wake ‘golden time.’ Ni rahisi kupata kazi muda mfupi baada ya kumaliza shule au kufukuzwa kazi kuliko kukaa nje ya ajira (kijiweni) kwa miaka sita au saba.

Kimsingi kuna maangalizo mengi katika mada hii ambayo watu wasiokuwa na ajira wanatakiwa kuzingatia lakini kwa uchache tutaangalia yale ambayo ni muhimu kufuatwa na watafuta ajira ili waweze kutumia ‘golden time’ vizuri na kuweza kuepuka madhara ya kisaikolojia na kutopata kazi.

KUTOTAHARUKI
Inashauriwa kuwa muda mfupi baada ya kufutwa kazi au kumaliza masomo na kukutana na vikwazo vya awali vya kukosa kazi, mhusika hatakiwi kuwa na taharuki kwa kuanza kunywa pombe, kustarehe, kuwa na msongo wa mawazo, bali anatakiwa kutulia na kuendelea kushikamana na wafanyakazi wenzake wa awali, wanafunzi waliomaliza naye shule na watu ambao wako kwenye mtandao wa kazi, ili kujiweka katika mazingira ya kuokoka ndani ya muda muafaka.

KUJITAMBUA
Mkosa ajira anatakiwa kujitambua kuwa yeye ni nani na kuhakikisha kuwa maisha yake yanakwenda kama yeye alivyo. Mhusika anatakiwa kutunza kumbukumbu zote za elimu yake kama vyeti na kuwa hai kila siku katika ujuzi wake. Pia haifai kuwa na aibu kwa kujiona duni, ni vema kuwa na imani kuwa kipindi cha kukosa ajira ni cha muda mfupi.

KUJITAMBULISHA
Muda wa awali ambao mtu atakuwa hana kazi ni muhimu sana kwake kufanya utambulisho kwa rafiki zake, ahakikishe kuwa watu wanaweza kuwasiliana naye kwa urahisi. Si busara kujifungia chumbani na kufunga simu, kufanya hivyo kunaweza kuwafanya rafiki zako washindwe kukupa dokezo za nafasi za kazi na hata kukusahau kabisa.

KUWA TAYARI
Unapokuwa katika ‘unemployment golden time’ni lazima uwe tayari wakati wote kwa kuanza kazi, isiwe unaambiwa kazi imepatikana unaanza kusema “sina vyeti, viko kwa bibi” muda wa dhahabu lazima utumike vizuri ili kutopoteza muda wa kujikomboa. Ni muhimu pia kuandaa CV yako na kuwa nayo kwenye kabati ili itakapohitajika usipoteze muda kuiandaa!

USIULEMAZE MWILI
Kuna watu ambao huchelewa kuamka au kushinda wamelala kwa sababu hawana kazi za kufanya, jambo ambalo ni hatari kwa afya. Hata kama ukosefu wa ajira unakuumiza kiasi gani usikubali kubweteka kwa kulala, utumikishe mwili pengine hata kwa kazi ambazo si za masilahi makubwa. Haifai kulazimisha sana ajira kwa kuwaganda mabosi.

USIKATE TAMAA
Kifupi hatua hizi ni muongozo wa kuweza kutumia muda wa dhahabu katika kupata kazi, hata hivyo mtu hatakiwi kukata tamaa ya kutafuta kazi ingawa ukweli utabaki kuwa kadiri unavyozidi kuchelewa kupata kazi kwa miaka mingi ndivyo anavyozidi kuweka mazingira magumu ya kuajiriwa. Hivyo ni bora ukahangaika mapema kwa kutumia uwezo na mbinu zote ili kuepuka kupotea katika ulimwengu wa ajira na kujikuta umeathirika kisaikolojia.

Sem comentários:

Publicar um comentário